MS Tech Home  /  BibleDatabase Home  /  Tell a Friend  / About MS Tech /Swahili New Testament Main Index

 

Revelation 9

[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22]

9:1 Kisha malaika wa tano akapiga tarumbeta yake. Nami nikaona nyota iliyokuwa imeanguka juu ya nchi kutoka mbinguni. Nayo ikapewa ufunguo wa shimo la Kuzimu.

9:2 Basi, nyota hiyo ikafungua shimo la Kuzimu, kukatoka moshi wa tanuru kubwa. Jua na anga vikatiwa giza kwa moshi huo wa Kuzimu.

9:3 Nzige wakatoka katika moshi huo, wakaingia duniani wakapewa nguvu kama ya ng`e.

9:4 Wakaamrishwa wasiharibu nyasi za nchi wala majani wala miti yoyote, bali wawaharibu wale tu ambao hawakupigwa mhuri wa Mungu katika paji la uso.

9:5 Nzige hao hawakuruhusiwa kuwaua watu, ila kuwatesa tu kwa muda wa miezi mitano. Maumivu watakayosababisha ni kama maumivu yanayompata mtu wakati anapoumwa na ng`e.

9:6 Muda huo watu watatafuta kifo lakini hawatakipata; watatamani kufa lakini kifo kitawakimbia.

9:7 Kwa kuonekana, nzige hao walikuwa kama farasi waliowekwa tayari kwa vita. Juu ya vichwa vyao walikuwa na taji zilizo kama za dhahabu, na nyuso zao zilikuwa kama za binadamu.

9:8 Nywele zao zilikuwa kama nywele za wanawake, na meno yao yalikuwa kama meno ya simba.

9:9 Vifua vyao vilikuwa vimefunikwa kitu kama ngao ya chuma. Sauti ya mabawa yao ilikuwa kama sauti ya msafara wa magari ya farasi wengi wanaokimbilia vitani.

9:10 Walikuwa na mikia na miiba kama ng`e, na kwa mikia hiyo, walikuwa na nguvu ya kuwadhuru watu kwa muda wa miezi mitano.

9:11 Tena wanaye mfalme anayewatawala, naye ndiye malaika wa kuzimu; jina lake kwa Kiebrania ni Abadoni, na kwa Kigiriki ni Apolioni, yaani mwangamizi.

9:12 Maafa ya kwanza yamepita; bado mengine mawili yanafuata.

9:13 Kisha malaika wa sita akapiga tarumbeta yake. Nami nikasikia sauti moja kutoka katika pembe nne za madhabahu ya dhahabu iliyokuwa mbele ya Mungu.

9:14 Sauti hiyo ikamwambia huyo malaika wa sita mwenye tarumbeta, "Wafungulie malaika wanne waliofungwa kwenye mto mkubwa `Eufrate!"`

9:15 Naye akawafungulia malaika hao wanne ambao walikuwa wametayarishwa kwa ajili ya saa hiyo ya siku ya mwezi huo, wa mwaka huohuo, kuua theluthi moja ya wanaadamu.

9:16 Nilisikia idadi ya majeshi wapanda farasi ilikuwa milioni mia mbili.

9:17 Hivi ndivyo nilivyowaona hao farasi na wapanda farasi katika hiyo njozi: Walikuwa na ngao vifuani zilizokuwa moto mtupu, zenye rangi ya samawati na njano kama kiberiti. Vichwa vya hao farasi vilikuwa kama vya simba; na moto, moshi, na kiberiti vilikuwa vinatoka kinywani mwao.

9:18 Theluthi moja ya wanaadamu waliuawa kwa mabaa hayo matatu yaani, moto, moshi na kiberiti, yaliyokuwa yanatoka katika vinywa vyao;

9:19 maana nguvu ya farasi hao ilikuwa vinywani mwao na katika mikia yao. Mikia yao ilikuwa na vichwa kama nyoka, na waliitumia hiyo kuwadhuru watu.

9:20 Wanaadamu wengine waliobaki ambao hawakuuawa na mabaa hayo, hawakugeuka na kuviacha vitu walivyokuwa wametengeneza kwa mikono yao wenyewe; bali wakaendelea kuabudu pepo, sanamu za dhahabu, fedha, shaba, mawe na miti, vitu ambavyo haviwezi kuona, kusikia wala kutembea.

9:21 Wala hawakutubu na kuacha kufanya mauaji, uchawi, uzinzi, na wizi.

 

Created with  FREE HTMLCompiler by Bibledatabase