MS Tech Home  /  BibleDatabase Home  /  Tell a Friend  / About MS Tech /Swahili New Testament Main Index

 

Matthew 8

[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22] [23] [24] [25] [26] [27]

8:1 Yesu aliposhuka kutoka mlimani, makundi mengi ya watu yalimfuata.

8:2 Basi, akaja mtu mmoja mwenye ukoma, akamsujudia akisema, "Bwana, ukitaka, waweza kunitakasa!"

8:3 Yesu akanyosha mkono wake, akamgusa na kusema, "Nataka! Takasika." Mara huyo mtu akapona ukoma wake.

8:4 Kisha Yesu akamwambia, "Sikiliza, usimwambie mtu yeyote, ila nenda ukajionyeshe kwa kuhani, na ukatoe sadaka iliyoamriwa na Mose kuwathibitishia kwamba umepona."

8:5 Yesu alipokuwa anaingia mjini Kafarnaumu, ofisa mmoja Mroma alimwendea, akamsihi

8:6 akisema, "Mheshimiwa, mtumishi wangu amelala nyumbani, mgonjwa wa kupooza na anaumwa sana."

8:7 Yesu akamwambia, "Nitakuja kumponya."

8:8 Huyo ofisa akamwambia, "Mheshimiwa, sistahili uingie nyumbani mwangu. Lakini sema tu neno, na mtumishi wangu atapona.

8:9 Maana, hata mimi niliye mtu chini ya mamlaka ya wengine, ninao askari chini yangu. Namwambia mmoja, `Nenda!` naye huenda; na mwingine, `Njoo!` naye huja; na mtumishi wangu, `Fanya kitu hiki!` naye hufanya."

8:10 Yesu aliposikia hayo, alistaajabu, akawaambia watu waliokuwa wanamfuata, "Kweli nawaambieni, sijapata kumwona mtu yeyote katika Israeli aliye na imani kama hii.

8:11 Basi, nawaambieni kwamba watu wengi watakuja kutoka mashariki na magharibi, nao wataketi karamuni pamoja na Abrahamu, Isaka na Yakobo katika Ufalme wa mbinguni.

8:12 Lakini wale ambao wangalipaswa kuwa katika Ufalme huo watatupwa nje, gizani, ambako watalia na kusaga meno."

8:13 Kisha Yesu akamwambia huyo ofisa Mroma, "Nenda nyumbani; na iwe kama ulivyoamini." Na mtumishi wake akapona saa ileile.

8:14 Yesu alifika nyumbani kwa Petro, akamkuta mama mkwe wa Petro amelala kitandani, ana homa kali.

8:15 Basi, Yesu akamgusa huyo mama mkono, na homa ikamwacha; akasimama, akamtumikia.

8:16 Ilipokuwa jioni, walimletea watu wengi waliokuwa wamepagawa na pepo; naye, kwa kusema neno tu, akawafukuza hao pepo. Aliwaponya pia watu wote waliokuwa wagonjwa.

8:17 Alifanya hivyo ili yale aliyosema nabii Isaya yatimie: "Yeye mwenyewe ameondoa udhaifu wetu, ameyachukua magonjwa yetu."

8:18 Yesu alipoona kundi la watu limemzunguka, aliwaamuru wanafunzi wake waende ng`ambo ya ziwa.

8:19 Mwalimu mmoja wa Sheria akamwendea, akamwambia, "Mwalimu, mimi nitakufuata kokote uendako."

8:20 Yesu akamjibu, "Mbweha wana mapango, na ndege wana viota; lakini Mwana wa Mtu hana mahali pa kupumzikia."

8:21 Kisha mtu mwingine miongoni mwa wanafunzi wake akamwambia, "Bwana, niruhusu kwanza niende nikamzike baba yangu."

8:22 Lakini Yesu akamwambia, "Nifuate! Waache wafu wazike wafu wao."

8:23 Yesu alipanda mashua, na wanafunzi wake wakaenda pamoja naye.

8:24 Ghafla, dhoruba kali ikatokea ziwani, hata mawimbi yakaanza kuifunika mashua. Yesu alikuwa amelala usingizi.

8:25 Wanafunzi wakamwendea, wakamwamsha wakisema, "Bwana, tuokoe, tunaangamia!"

8:26 Yesu akawaambia, "Enyi watu wenye imani haba; mbona mnaogopa?" Basi, akainuka, akazikemea pepo na mawimbi; kukawa shwari kabisa.

8:27 Watu wakashangaa, wakasema, "Ni mtu wa namna gani huyu? Hata pepo na mawimbi vinamtii!"

8:28 Yesu alifika katika nchi ya Wagerasi,*fb* ng`ambo ya ziwa, na huko watu wawili waliopagawa na pepo wakakutana naye wakitokea makaburini. Watu hawa walikuwa wenye kutisha mno, hata hakuna mtu aliyethubutu kupita katika njia hiyo.

8:29 Nao wakaanza kupiga kelele, "Una shauri gani nasi, wewe Mwana wa Mungu? Je, umekuja kututesa kabla ya wakati wake?"

8:30 Karibu na mahali hapo kulikuwa na nguruwe wengi wakichungwa.

8:31 Basi, hao pepo wakamsihi, "Ikiwa utatutoa, basi uturuhusu tuwaingie nguruwe wale."

8:32 Yesu akawaambia, "Haya, nendeni." Hapo wakawatoka watu hao, wakawaingia nguruwe. Kundi lote la nguruwe likaporomoka kwenye ule mteremko mkali, likatumbukia ziwani; nguruwe wote wakafa maji.

8:33 Wachungaji wa hao nguruwe walikimbia, wakaenda mjini. Huko walitoa habari zote na mambo yaliyowapata wale watu waliokuwa wamepagawa.

8:34 Basi, watu wote katika mji ule walitoka, wakamwendea Yesu; na walipomwona, wakamsihi aondoke katika nchi yao.

 

Created with  FREE HTMLCompiler by Bibledatabase