MS Tech Home  /  BibleDatabase Home  /  Tell a Friend  / About MS Tech /Swahili New Testament Main Index

 

Matthew 24

[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22] [23] [24] [25] [26] [27]

24:1 Yesu alitoka Hekaluni, na alipokuwa akienda zake, wanafunzi wake walimwendea, wakamwonyesha majengo ya Hekalu.

24:2 Yesu akawaambia, "Sawa, mnaweza kuyatazama haya yote! Kweli nawaambieni, hakuna hata jiwe moja litakalosalia hapa juu ya lingine; kila kitu kitaharibiwa."

24:3 Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni, wanafunzi walimwendea faraghani, wakamwuliza, "Twambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonyesha kuja kwako na mwisho wa nyakati?"

24:4 Yesu akawajibu, "Jihadharini msije mkadanganywa na mtu.

24:5 Maana wengi watatokea na kulitumia jina langu wakisema: `Mimi ndiye Kristo,` nao watawapotosha watu wengi.

24:6 Mtasikia juu ya vita na fununu za vita; lakini msifadhaike, maana hayo hayana budi kutokea, lakini mwisho wenyewe ungali bado.

24:7 Taifa moja litapigana na taifa lingine; ufalme mmoja utapigana na ufalme mwingine. Hapa na pale patakuwa na njaa na mitetemeko ya ardhi.

24:8 Yote hayo ni kama mwanzo wa maumivu ya kujifungua mtoto.

24:9 "Kisha watawatoeni ili mteswe na kuuawa. Mataifa yote yatawachukieni kwa ajili ya jina langu.

24:10 Tena, wengi wataiacha imani yao, watasalitiana na kuchukiana.

24:11 Watatokea manabii wengi wa uongo watakaowapotosha watu wengi.

24:12 Kwa sababu ya ongezeko la uhalifu, upendo wa watu wengi utafifia.

24:13 Lakini atakayevumilia mpaka mwisho, ataokoka.

24:14 Ila, kabla ya mwisho kufika, hii Habari Njema ya Ufalme wa Mungu itahubiriwa ulimwenguni kote kama ushuhuda kwa mataifa yote.

24:15 "Basi, mtakapoona `Chukizo Haribifu` lililonenwa na nabii Danieli limesimama mahali patakatifu, (msomaji na atambue maana yake),

24:16 hapo, walioko Yudea na wakimbilie milimani.

24:17 Aliye juu ya paa la nyumba yake asishuke kuchukua kitu nyumbani mwake.

24:18 Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake.

24:19 Ole wao kina mama waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo!

24:20 Ombeni ili kukimbia kwenu kusiwe siku za baridi au siku ya Sabato!

24:21 Maana wakati huo kutakuwa na dhiki kuu ambayo haijapata kuwako tangu mwanzo wa ulimwengu mpaka leo, wala haitapata kutokea tena.

24:22 Kama siku hizo hazingalipunguzwa, hakuna binadamu yeyote ambaye angeokoka; lakini siku hizo zitapunguzwa kwa ajili ya wale walioteuliwa.

24:23 "Basi, mtu akiwaambieni siku hizo: `Kristo yuko hapa` au `Yuko pale,` msimsadiki.

24:24 Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo. Watafanya ishara kubwa na maajabu ya kuweza kuwapotosha ikiwezekana hata wateule wa Mungu.

24:25 Sikilizeni, nimekwisha kuwaonya kabla ya wakati.

24:26 Basi, wakiwaambieni, `Tazameni, yuko jangwani,` msiende huko; au, `Tazameni, amejificha ndani,` msisadiki;

24:27 maana, kama vile umeme uangazavyo toka mashariki hadi magharibi, ndivyo kutakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu.

24:28 Pale ulipo mzoga, ndipo watakapokusanyika tai.

24:29 "Mara baada ya dhiki ya siku hizo, jua litatiwa giza, mwezi hautaangaza, nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa.

24:30 Kisha, ishara ya Mwana wa Mtu itaonekana angani, na hapo makabila yote duniani yatalalamika; watamwona Mwana wa Mtu akija juu ya mawingu ya angani mwenye nguvu na utukufu mwingi.

24:31 Naye atawatuma malaika wake wenye tarumbeta la kuvuma sana, nao watawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, toka mwisho huu wa mbingu hadi mwisho huu.

24:32 "Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.

24:33 Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo haya yote yakitendeka, jueni kwamba yuko karibu sana.*fk*

24:34 Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia.

24:35 Naam, mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

24:36 "Lakini, juu ya siku au saa hiyo, hakuna mtu ajuaye itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana, ila Baba peke yake ndiye ajuaye.

24:37 Kwa maana kama ilivyokuwa nyakati za Noa, ndivyo itakavyokuwa kuja kwake Mwana wa Mtu.

24:38 Maana nyakati hizo, kabla ya gharika kuu, watu walikuwa wakila na kunywa, wakioa na kuolewa, mpaka Noa alipoingia ndani ya ile safina.

24:39 Hawakujua kuna nini mpaka ile gharika ilipotokea, ikawakumba wote. Ndivyo itakavyokuwa wakati Mwana wa Mtu atakapokuja.

24:40 Wakati huo watu wawili watakuwa shambani; mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.

24:41 Kina mama wawili watakuwa wanasaga nafaka, mmoja atachukuliwa na mwingine ataachwa.

24:42 Basi, kesheni, kwa maana hamjui siku atakayokuja Bwana wenu.

24:43 Lakini kumbukeni jambo hili: kama mwenye nyumba angejua siku mwizi atakapofika, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe.

24:44 Kwa hiyo, nanyi pia muwe tayari, kwa maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia."

24:45 Yesu akaendelea kusema, "Ni nani basi mtumishi mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watu wake, awape chakula kwa wakati wake?

24:46 Heri mtumishi yule ambaye bwana wake atakapokuja atamkuta akifanya hivyo.

24:47 Kweli nawaambieni, atamweka mtumishi huyo aisimamie mali yake yote.

24:48 Lakini kama mtumishi mbaya akijisemea moyoni: `Bwana wangu anakawia kurudi,`

24:49 kisha akaanza kuwapiga watumishi wenzake, akaanza kula na kunywa pamoja na walevi,

24:50 bwana wake atakuja siku asiyoitazamia na saa asiyoijua.

24:51 Atamkatilia mbali na kumweka kundi moja na wanafiki. Huko kutakuwa na kilio na kusaga meno.

 

Created with  FREE HTMLCompiler by Bibledatabase