MS Tech Home  /  BibleDatabase Home  /  Tell a Friend  / About MS Tech /Swahili New Testament Main Index

 

Mark 3

[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16]

3:1 Yesu aliingia tena katika sunagogi na mle ndani mlikuwa na mtu aliyekuwa na mkono uliopooza.

3:2 Humo baadhi ya watu walimngojea amponye mtu huyo siku ya sabato ili wapate kumshtaki.

3:3 Yesu akamwambia huyo mtu aliyekuwa na mkono uliopooza, "Njoo hapa katikati."

3:4 Kisha, akawauliza, "Je, ni halali siku ya Sabato kutenda jambo jema au kutenda jambo baya; kuokoa maisha au kuua?" Lakini wao hawakusema neno.

3:5 Hapo akawatazama wote kwa hasira, akaona huzuni kwa sababu ya ugumu wa mioyo yao. Kisha akamwambia huyo mtu, "Nyosha mkono wako!" Naye akaunyosha mkono wake, ukawa mzima tena.

3:6 Mara Mafarisayo wakatoka nje, wakafanya shauri pamoja na watu wa kikundi cha Herode jinsi ya kumwangamiza Yesu.

3:7 Yesu aliondoka hapo pamoja na wanafunzi wake, akaenda kando ya ziwa, na umati wa watu ukamfuata. Watu hao walikuwa wametoka Yerusalemu, Yudea,

3:8 Idumea, ng`ambo ya mto Yordani, Tiro na Sidoni. Watu hao wengi walimwendea Yesu kwa sababu ya kusikia mambo mengi aliyokuwa ameyatenda.

3:9 Yesu akawaambia wanafunzi wake wamtayarishie mashua moja, ili umati wa watu usije ukamsonga.

3:10 Alikuwa amewaponya watu wengi, na wagonjwa wote wakawa wanamsonga ili wapate kumgusa.

3:11 Na watu waliokuwa wamepagawa na pepo wachafu walipomwona, walijitupa chini mbele yake na kupaaza sauti, "Wewe ni Mwana wa Mungu!"

3:12 Lakini Yesu akawaamuru kwa ukali wasimjulishe kwa watu.

3:13 Yesu alipanda kilimani, akawaita wale aliowataka. Basi, wakamwendea,

3:14 naye akawateua watu kumi na wawili ambao aliwaita mitume,*fb* wakae naye, awatume kuhubiri

3:15 na wawe na mamlaka ya kuwafukuza pepo.

3:16 Basi, hao kumi na wawili walioteuliwa ndio hawa: Simoni (ambaye Yesu alimpa jina, Petro),

3:17 Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo (Yesu aliwapa hawa ndugu wawili jina Boanerge, maana yake "wanangurumo"),

3:18 Andrea na Filipo, Batholomayo, Mathayo, Thoma, Yakobo mwana wa Alfayo, Thadayo, Simoni Mkanani na

3:19 Yuda Iskarioti ambaye alimsaliti Yesu.

3:20 Kisha Yesu alikwenda nyumbani. Umati wa watu ukakusanyika tena, hata Yesu na wafuasi wake wasiweze kupata nafasi ya kula chakula.

3:21 Basi, watu wa jamaa yake walipopata habari hiyo wakatoka kwenda kumchukua maana walikuwa wanasema kwamba amepatwa na wazimu.

3:22 Nao walimu wa Sheria waliokuwa wametoka Yerusalemu, wakasema, "Ana Beelzebuli! Tena, anawafukuza pepo kwa nguvu ya mkuu wa pepo."

3:23 Hapo Yesu akawaita, akawaambia kwa mifano,"Shetani anawezaje kumfukuza Shetani?

3:24 Ikiwa utawala mmoja umegawanyika makundimakundi yanayopigana, utawala huo hauwezi kudumu.

3:25 Tena, ikiwa jamaa moja imegawanyika makundimakundi yanayopingana, jamaa hiyo itaangamia.

3:26 Ikiwa basi, utawala wa Shetani umegawanyika vikundivikundi hauwezi kudumu, bali utaangamia kabisa.

3:27 "Hakuna mtu awezaye kuivamia nyumba ya mtu mwenye nguvu na kumnyang`anya mali yake, isipokuwa kwanza amemfunga huyo mtu mwenye nguvu; hapo ndipo atakapoweza kumnyang`anya mali yake.

3:28 "Kweli nawaambieni, watu watasamehewa dhambi zao zote na kufuru zao zote;

3:29 lakini anayesema mabaya dhidi ya Roho Mtakatifu, hatasamehewa kamwe; ana hatia ya dhambi ya milele."

3:30 Yesu alisema hivyo kwa sababu walikuwa wanasema, "Ana pepo mchafu.")

3:31 Mama yake Yesu na ndugu zake walifika hapo, wakasimama nje, wakampelekea ujumbe kutaka kumwona.

3:32 Umati wa watu ulikuwa umekaa hapo kumzunguka. Basi, wakamwambia, "Mama yako na ndugu zako wako nje, wanataka kukuona."

3:33 Yesu akawaambia, "Mama yangu na ndugu zangu ni kina nani?"

3:34 Hapo akawatazama watu waliokuwa wamemzunguka, akasema, "Tazameni! Hawa ndio mama yangu na ndugu zangu.

3:35 Mtu yeyote anayefanya anayotaka Mungu, huyo ndiye kaka yangu, dada yangu na mama yangu."

 

Created with  FREE HTMLCompiler by Bibledatabase