MS Tech Home  /  BibleDatabase Home  /  Tell a Friend  / About MS Tech /Swahili New Testament Main Index

 

Mark 13

[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16]

13:1 Yesu alipokuwa anatoka Hekaluni, mmoja wa wanafunzi wake alimwambia, "Mwalimu, tazama jinsi mawe haya na majengo haya yalivyo ya ajabu!"

13:2 Yesu akamwambia, "Je, unayaona majengo haya makubwa? Hakuna hata jiwe moja litakalosalia juu ya lingine; kila kitu kitabomolewa."

13:3 Yesu alipokuwa ameketi juu ya mlima wa Mizeituni akielekea Hekalu, Petro, Yakobo, Yohane na Andrea wakamwuliza kwa faragha,

13:4 "Twambie mambo haya yatatukia lini? Ni ishara gani itakayoonyesha kwamba mambo haya karibu yatimizwe?"

13:5 Yesu akaanza kuwaambia, "Jihadharini msije mkadanganywa na mtu.

13:6 Maana wengi watakuja wakilitumia jina langu, wakisema, `Mimi ndiye!` nao watawapotosha watu wengi.

13:7 Mtakaposikia juu ya vita na fununu za vita, msifadhaike. Mambo hayo lazima yatokee, lakini mwisho wenyewe ungali bado.

13:8 Taifa moja litapigana na taifa lingine; utawala mmoja utapigana na utawala mwingine; kila mahali kutakuwa na mitetemeko ya ardhi na njaa. Mambo haya ni kama tu maumivu ya kwanza ya kujifungua mtoto.

13:9 "Lakini ninyi jihadharini. Maana watu watawapelekeni mahakamani, na kuwapigeni katika masunagogi. Mtapelekwa mbele ya watawala na wafalme kwa sababu yangu ili mpate kunishuhudia kwao.

13:10 Lakini lazima kwanza Habari Njema ihubiriwe kwa mataifa yote.

13:11 Nao watakapowatieni nguvuni na kuwapeleka mahakamani, msiwe na wasiwasi juu ya yale mtakayosema; saa ile itakapofika, semeni chochote mtakachopewa, maana si ninyi mtakaosema, bali Roho Mtakatifu.

13:12 Ndugu atamsaliti ndugu yake auawe; baba atamsaliti mwanae; watoto watawashambulia wazazi wao na kuwaua.

13:13 Watu wote watawachukieni ninyi kwa sababu ya jina langu. Lakini atakayevumilia mpaka mwisho ndiye atakayeokolewa.

13:14 "Mtakapoona `Chukizo Haribifu` limesimama mahali ambapo si pake, (msomaji na atambue maana yake!) Hapo watu walioko Yudea wakimbilie milimani.

13:15 Mtu aliye juu ya paa la nyumba asishuke kuingia nyumbani mwake kuchukua kitu.

13:16 Aliye shambani asirudi nyuma kuchukua vazi lake.

13:17 Ole wao waja wazito na wanaonyonyesha siku hizo!

13:18 Ombeni ili mambo hayo yasitukie nyakati za baridi.

13:19 Maana wakati huo kutakuwa na dhiki ambayo haijatokea tangu Mungu alipoumba ulimwengu mpaka leo, wala haitatokea tena.

13:20 Kama Bwana asingepunguza siku hizo, hakuna binadamu ambaye angeokolewa. Lakini kwa ajili ya wateule wake, Bwana amezipunguza siku hizo.

13:21 "Basi mtu akiwaambieni, `Tazama, Kristo yupo hapa!` au `Yupo pale!` msimsadiki.

13:22 Maana watatokea kina Kristo wa uongo na manabii wa uongo, watafanya ishara na maajabu, ili kuwapotosha wateule wa Mungu, kama ikiwezekana.

13:23 Lakini ninyi jihadharini. Mimi nimewaambieni mambo yote kabla hayajatokea.

13:24 "Basi, siku hizo baada ya dhiki hiyo, jua litatiwa giza na mwezi hautaangaza.

13:25 Nyota zitaanguka kutoka angani, na nguvu za mbingu zitatikiswa.

13:26 Hapo watamwona Mwana wa Mtu akija katika mawingu kwa nguvu nyingi na utukufu.

13:27 Kisha atawatuma malaika wake; atawakusanya wateule wake kutoka pande zote nne za dunia, kutoka mwisho wa dunia mpaka mwisho wa mbingu.

13:28 "Kwa mtini jifunzeni mfano huu: Mara tu matawi yake yanapoanza kuwa laini na kuchanua majani, mnajua kwamba wakati wa kiangazi umekaribia.

13:29 Hali kadhalika nanyi mtakapoona mambo hayo yakitendeka, jueni kwamba Mwana wa Mtu yuko karibu sana.

13:30 Nawaambieni kweli, kizazi hiki hakitapita kabla ya mambo hayo yote kutukia.

13:31 Mbingu na dunia zitapita, lakini maneno yangu hayatapita kamwe.

13:32 "Lakini hakuna mtu ajuaye siku au saa hiyo itakuja lini; wala malaika wa mbinguni, wala Mwana; Baba peke yake ndiye ajuaye.

13:33 Muwe waangalifu na kesheni, maana hamjui wakati huo utafika lini.

13:34 Itakuwa kama mtu anayeondoka nyumbani kwenda safari akiwaachia watumishi wake madaraka, kila mmoja na kazi yake; akamwambia mlinzi wa mlango awe macho.

13:35 Kesheni, basi, kwa maana hamjui mwenye nyumba atarudi lini; huenda ikawa jioni, usiku wa manane, alfajiri au asubuhi.

13:36 Kesheni ili akija ghafla asije akawakuta mmelala.

13:37 Ninayowaambieni ninyi, nawaambia wote: Kesheni!"

 

Created with  FREE HTMLCompiler by Bibledatabase