MS Tech Home  /  BibleDatabase Home  /  Tell a Friend  / About MS Tech /Swahili New Testament Main Index

 

Mark 1

[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16]

1:1 Habari Njema ya Yesu Kristo, Mwana wa Mungu.*fa*

1:2 Ilianza kama ilivyoandikwa katika kitabu cha nabii Isaya: "Tazama, namtuma mjumbe wangu akutangulie; yeye atakutayarishia njia yako.

1:3 Sauti ya mtu imesikika jangwani: `Mtayarishieni Bwana njia yake, nyoosheni mapito yake."`

1:4 Yohane Mbatizaji alitokea jangwani, akahubiri kwamba ni lazima watu watubu na kubatizwa ili Mungu awasamehe dhambi zao.

1:5 Watu kutoka sehemu zote za Yudea na wenyeji wote wa Yerusalemu walimwendea, wakaziungama dhambi zao, naye akawabatiza katika mto Yordani.

1:6 Yohane alikuwa amevaa vazi lililofumwa kwa manyoya ya ngamia, na mkanda wa ngozi kiunoni mwake. Chakula chake kilikuwa nzige na asali ya mwituni.

1:7 Naye alihubiri akisema, "Baada yangu anakuja mwenye uwezo zaidi kuliko mimi, ambaye mimi sistahili hata kuinama na kufungua kamba za viatu vyake.

1:8 Mimi ninawabatiza kwa maji, lakini yeye atawabatiza kwa Roho Mtakatifu."

1:9 Siku hizo, Yesu alifika kutoka Nazareti, mji wa Galilaya, akabatizwa na Yohane katika mto Yordani.

1:10 Mara tu alipotoka majini, aliona mbingu zimefunguliwa, na Roho akishuka juu yake kama njiwa.

1:11 Sauti ikasikika kutoka mbinguni: "Wewe ni Mwanangu mpendwa, nimependezwa nawe."

1:12 Mara akaongozwa na Roho kwenda jangwani,

1:13 akakaa huko siku arubaini akijaribiwa na Shetani. Alikuwa huko pamoja na wanyama wa porini, nao malaika wakawa wanamtumikia.

1:14 Yohane alipokwisha fungwa gerezani, Yesu alikwenda Galilaya, akahubiri Habari Njema ya Mungu, akisema,

1:15 "Wakati umetimia, na Ufalme wa Mungu umekaribia. Tubuni na kuiamini Habari Njema!"

1:16 Alipokuwa anapita kando ya ziwa Galilaya, aliwaona wavuvi wawili: Simoni na Andrea ndugu yake wakivua samaki kwa wavu.

1:17 Yesu akawaambia, "Nifuateni nami nitawafanya ninyi wavuvi wa watu."

1:18 Mara wakaziacha nyavu zao, wakamfuata.

1:19 Alipokwenda mbele kidogo, aliwaona Yakobo na Yohane, wana wa Zebedayo. Nao pia walikuwa ndani ya mashua yao wakizitengeneza nyavu zao.

1:20 Yesu akawaita mara, nao wakamwacha baba yao Zebedayo katika mashua pamoja na wafanyakazi, wakamfuata.

1:21 Wakafika mjini Kafarnaumu, na mara ilipofika Sabato, Yesu akaingia katika Sunagogi, akaanza kufundisha.

1:22 Watu wote waliomsikia walishangazwa na mafundisho yake, maana hakuwa anafundisha kama walimu wao wa Sheria, bali kama mtu mwenye mamlaka.

1:23 Mara akatokea mle ndani ya sunagogi mtu mmoja mwenye pepo mchafu,

1:24 akapaaza sauti, "Una nini nasi, wewe Yesu wa Nazareti? Je, umekuja kutuangamiza? Najua wewe ni nani: wewe ni Mtakatifu wa Mungu!"

1:25 Yesu akamkemea, "Nyamaza! Mtoke mtu huyu."

1:26 Basi, huyo pepo mchafu akamtikisatikisa mtu huyo, kisha akalia kwa sauti kubwa, akamtoka.

1:27 Watu wote wakashangaa, wakaulizana, "Ni mambo gani haya? Je, ni mafundisho mapya? Mtu huyu anayo mamlaka ya kuamuru hata pepo wachafu, nao wanamtii!"

1:28 Habari za Yesu zikaenea upesi kila mahali katika wilaya ya Galilaya.

1:29 Wakatoka katika sunagogi, wakaenda moja kwa moja hadi nyumbani kwa Simoni na Andrea; Yakobo na Yohane walikwenda pamoja nao.

1:30 Basi, mama mmoja, mkwewe Simoni, alikuwa kitandani ana homa kali. Wakamwarifu Yesu mara alipowasili.

1:31 Yesu akamwendea huyo mama, akamshika mkono, akamwinua. Na ile homa ikamwacha, akaanza kuwatumikia.

1:32 Jioni, jua lilipokwisha tua, wakamletea Yesu wagonjwa wote na watu waliopagawa na pepo.

1:33 Watu wote wa mji ule wakakusanyika nje ya mlango.

1:34 Naye Yesu akawaponya watu wengi waliokuwa na magonjwa mbalimbali; aliwafukuza pepo wengi, lakini hakuwaruhusu kusema kitu maana walikuwa wanamjua yeye ni nani.

1:35 Kesho yake, kabla ya mapambazuko, Yesu alitoka, akaenda mahali pa faragha kusali.

1:36 Simoni na wenzake wakaenda kumtafuta.

1:37 Walipomwona wakamwambia, "Kila mtu anakutafuta."

1:38 Yesu akawaambia, "Twendeni katika miji mingine ya jirani nikahubiri huko pia, maana nimekuja kwa sababu hiyo."

1:39 Basi, akaenda kila mahali Galilaya akihubiri katika masunagogi na kufukuza pepo.

1:40 Mtu mmoja mwenye ukoma alimwendea Yesu, akapiga magoti, akamwomba, "Ukitaka, waweza kunitakasa!"

1:41 Yesu akamwonea huruma, akanyosha mkono wake, akamgusa na kumwambia, "Nataka, takasika!"

1:42 Mara ukoma ukamwacha mtu huyo, akatakasika.

1:43 Kisha Yesu akamwambia aende zake upesi na kumwonya vikali,

1:44 "Usimwambie mtu yeyote jambo hili, ila nenda ukajionyeshe kwa kuhani; kisha utoe sadaka kwa ajili ya kutakasika kwako kama alivyoamuru Mose, iwe uthibitisho kwao kwamba umepona."

1:45 Lakini huyo mtu akaenda, akaanza kueneza habari hiyo kila mahali na kusema mambo mengi hata Yesu hakuweza tena kuingia katika mji wowote waziwazi; ikamlazimu kukaa nje, mahali pa faragha. Hata hivyo, watu wakamwendea kutoka kila upande.

 

Created with  FREE HTMLCompiler by Bibledatabase