MS Tech Home  /  BibleDatabase Home  /  Tell a Friend  / About MS Tech /Swahili New Testament Main Index

 

Luke 18

[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22] [23] [24]

18:1 Basi, Yesu aliwasimulia mfano kuonyesha kwamba ni lazima kusali daima bila kukata tamaa.

18:2 Alisema: "Katika mji mmoja kulikuwa na hakimu ambaye hakuwa anamcha Mungu wala kumjali binadamu.

18:3 Katika mji huohuo, kulikuwa pia na mama mmoja mjane, ambaye alimwendea huyo hakimu mara nyingi akimwomba amtetee apate haki yake kutoka kwa adui yake.

18:4 Kwa muda mrefu huyo hakimu hakupenda kumtetea huyo mjane; lakini, mwishowe akajisemea: `Ingawa mimi simchi Mungu wala simjali binadamu,

18:5 lakini kwa vile huyu mjane ananisumbua, nitamtetea; la sivyo ataendelea kufika hapa, na mwisho atanichosha kabisa!"`

18:6 Basi, Bwana akaendelea kusema, "Sikieni jinsi alivyosema huyo hakimu mbaya.

18:7 Je, ndio kusema Mungu hatawatetea wale aliowachagua, ambao wanamlilia mchana na usiku? Je, atakawia kuwasikiliza?

18:8 Nawaambieni atawatetea upesi. Hata hivyo, je, kutakuwako na imani duniani wakati Mwana wa Mtu atakapokuja?"

18:9 Halafu Yesu aliwaambia pia mfano wa wale ambao walijiona kuwa wema na kuwadharau wengine.

18:10 "Watu wawili walipanda kwenda Hekaluni kusali: mmoja Mfarisayo, na mwingine mtoza ushuru.

18:11 Huyo Mfarisayo akasimama, akasali kimoyomoyo: `Ee Mungu, nakushukuru kwa vile mimi si kama watu wengine: walafi, wadanganyifu au wazinzi. Nakushukuru kwamba mimi si kama huyu mtoza ushuru.

18:12 Nafunga mara mbili kwa juma, natoa zaka sehemu ya kumi ya pato langu.`

18:13 Lakini yule mtoza ushuru, akiwa amesimama kwa mbali bila hata kuinua macho yake mbinguni, ila tu akijipiga kifua kwa huzuni, alisema: `Ee Mungu, unionee huruma mimi mwenye dhambi.`

18:14 Nawaambieni, huyu mtoza ushuru alirudi nyumbani akiwa amesamehewa. Lakini yule mwingine, sivyo. Kwa maana kila anayejikweza atashushwa, na kila anayejishusha atakwezwa."

18:15 Watu walimletea Yesu watoto wadogo ili awawekee mikono yake. Wanafunzi walipowaona, wakawazuia kwa maneno makali.

18:16 Lakini Yesu akawaita kwake akisema: "Waacheni hao watoto waje kwangu, wala msiwazuie, kwa maana Ufalme wa Mungu ni kwa ajili ya watu kama hawa.

18:17 Nawaambieni kweli, mtu yeyote asiyeupokea Ufalme wa Mungu kama mtoto mdogo, hataingia katika Ufalme huo."

18:18 Kiongozi mmoja, Myahudi, alimwuliza Yesu, "Mwalimu mwema, nifanye nini ili niweze kuupata uzima wa milele?"

18:19 Yesu akamwambia, "Mbona waniita mwema? Hakuna aliye mwema ila Mungu peke yake.

18:20 Unazijua amri: `Usizini; usiue; usiibe; usitoe ushahidi wa uongo; waheshimu baba yako na mama yako."`

18:21 Yeye akasema, "Hayo yote nimeyazingatia tangu ujana wangu."

18:22 Yesu aliposikia hayo akamwambia, "Unatakiwa bado kufanya kitu kimoja: uza kila ulicho nacho, wagawie maskini, na hivyo utakuwa na hazina yako mbinguni; halafu njoo unifuate."

18:23 Lakini huyo mtu aliposikia hayo, alihuzunika sana kwa sababu alikuwa tajiri sana.

18:24 Yesu alipoona akihuzunika hivyo, akasema, "Jinsi gani ilivyo vigumu kwa matajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu!

18:25 Naam, ni rahisi zaidi kwa ngamia kupita katika tundu la sindano, kuliko tajiri kuingia katika Ufalme wa Mungu."

18:26 Wale watu waliposikia hayo, wakasema, "Nani basi, atakayeokolewa?"

18:27 Yesu akajibu, "Yasiyowezekana kwa binadamu, yanawezekana kwa Mungu."

18:28 Naye Petro akamwuliza, "Na sisi je? Tumeacha vitu vyote tukakufuata!"

18:29 Yesu akawaambia, "Kweli nawaambieni, mtu yeyote aliyeacha nyumba au mke au kaka au wazazi au watoto kwa ajili ya Ufalme wa Mungu,

18:30 atapokea mengi zaidi wakati huu wa sasa, na kupokea uzima wa milele wakati ujao."

18:31 Yesu aliwachukua kando wale kumi na wawili, akawaambia, "Sikilizeni! Tunakwenda Yerusalemu na huko kila kitu kilichoandikwa na manabii kuhusu Mwana wa Mtu kitakamilishwa.

18:32 Kwa maana atakabidhiwa kwa watu wa mataifa nao watamtendea vibaya na kumtemea mate.

18:33 Watampiga mijeledi, watamuua; lakini siku ya tatu atafufuka."

18:34 Lakini wao hawakuelewa hata kidogo jambo hilo; walikuwa wamefichwa maana ya maneno hayo, na hawakutambua yaliyosemwa.

18:35 Wakati Yesu alipokaribia Yeriko, kulikuwa na mtu mmoja kipofu ameketi njiani akiomba.

18:36 Aliposikia umati wa watu ukipita aliuliza, "Kuna nini?"

18:37 Wakamwambia, "Yesu wa Nazareti anapita."

18:38 Naye akapaza sauti akisema, "Yesu, Mwana wa Daudi, nihurumie!"

18:39 Wale watu waliotangulia wakamkemea wakimwambia anyamaze; lakini yeye akazidi kupaza sauti: "Mwana wa Daudi, nihurumie;"

18:40 Yesu alisimama, akaamuru wamlete mbele yake. Yule kipofu alipofika karibu, Yesu akamwuliza,

18:41 "Unataka nikufanyie nini?" Naye akamjibu, "Bwana, naomba nipate kuona tena."

18:42 Yesu akamwambia, "Ona! Imani yako imekuponya."

18:43 Na mara yule aliyekuwa kipofu akapata kuona, akamfuata Yesu akimtukuza Mungu. Watu wote walipoona hayo, wakamsifu Mungu.

 

Created with  FREE HTMLCompiler by Bibledatabase