![]() |
![]() |
|
MS Tech Home / BibleDatabase Home / Tell a Friend / About MS Tech / |
Luke 12
[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21] [22] [23] [24]
12:1 Wakati watu kwa maelfu walipokuwa wamekusanyika hata wakawa wanakanyagana, Yesu aliwaambia kwanza wanafunzi wake, "Jihadharini na chachu ya Mafarisayo, yaani unafiki.
12:2 Kila kilichofunikwa kitafunuliwa, kila kilichofichika kitafichuliwa.
12:3 Kwa hiyo, kila mliyosema gizani, watu watayasikia katika mwanga, na kila mliyonong`ona faraghani milango imefungwa, yatatangazwa juu ya nyumba.
12:4 "Nawaambieni ninyi rafiki zangu: msiwaogope wale wanaoua mwili, wasiweze kufanya kitu kingine zaidi.
12:5 Nitawaonyesheni yule ambaye ni lazima kumwogopa: mwogopeni yule ambaye baada ya kuua ana uwezo wa kumtupa mtu katika moto wa Jehanamu. Naam, ninawaambieni, mwogopeni huyo.
12:6 Inajulikana kwamba shomoro watano huuzwa kwa senti kumi, au sivyo? Lakini mbele ya Mungu hasahauliki hata mmoja.
12:7 Lakini hata nywele za vichwa vyenu zimehesabiwa zote. Msiogope, basi, ninyi mna thamani zaidi kuliko shomoro wengi!
12:8 "Nawaambieni kweli, kila mtu anayekiri hadharani kwamba yeye ni wangu, Mwana wa Mtu naye atakiri mbele ya malaika wa Mungu kwamba mtu huyo ni wake.
12:9 Lakini, mtu yeyote anayenikana mbele ya watu, naye atakanwa mbele ya malaika wa Mungu.
12:10 "Yeyote anayesema neno la kumpinga Mwana wa Mtu atasamehewa; lakini anayemkufuru Roho Mtakatifu hatasamehewa.
12:11 "Watakapowapeleka ninyi mbele ya masunagogi na mbele ya wakuu na watawala msiwe na wasiwasi juu ya jinsi mtakavyojitetea au jinsi mtakavyosema.
12:12 Kwa maana wakati huo Roho Mtakatifu atawafundisheni kile mnachopaswa kusema."
12:13 Mtu mmoja katika ule umati wa watu akamwambia, "Mwalimu, mwambie ndugu yangu tugawane urithi aliotuachia baba."
12:14 Yesu akamjibu, "Rafiki, ni nani aliyeniweka mimi mwamuzi au msuluhishi kati yenu?"
12:15 Basi, akawaambia wote, "Jihadharini na kila aina ya tamaa; maana uzima wa mtu hautegemei wingi wa vitu alivyo navyo."
12:16 Kisha akawaambia mfano: "Kulikuwa na tajiri mmoja ambaye shamba lake lilizaa mavuno mengi.
12:17 Tajiri huyo akafikiri moyoni mwake: `Nitafanyaje nami sina mahali pa kuhifadhia mavuno yangu?
12:18 Nitafanya hivi: nitabomoa ghala zangu na kujenga kubwa zaidi, na humo nitahifadhi mavuno yangu yote na mali yangu.
12:19 Hapo nitaweza kuiambia roho yangu: sasa unayo akiba ya matumizi kwa miaka na miaka. Ponda mali, ule, unywe na kufurahi.`
12:20 Lakini Mungu akamwambia: `Mpumbavu wewe; leo usiku roho yako itachukuliwa. Na vitu vile vyote ulivyojilundikia vitakuwa vya nani?"`
12:21 Yesu akamaliza kwa kusema "Ndivyo ilivyo kwa mtu anayejilundikia mali kwa ajili yake mwenyewe, lakini si tajiri mbele ya Mungu."
12:22 Kisha Yesu akawaambia wanafunzi wake, "Kwa sababu hiyo nawaambieni, msiwe na wasiwasi juu ya chakula mnachohitaji ili kuishi, wala juu ya mavazi mnayohitaji kwa ajili ya miili yenu.
12:23 Kwa sababu uzima ni bora kuliko chakula, na mwili ni bora kuliko mavazi.
12:24 Chukueni kwa mfano, kunguru: hawapandi, hawavuni wala hawana ghala yoyote. Hata hivyo, Mungu huwalisha. Ninyi mna thamani zaidi kuliko ndege!
12:25 Ni nani kati yenu kwa kuwa na wasiwasi anaweza kuongeza urefu wa maisha yake?
12:26 Basi, kama hamwezi kufanya jambo dogo kama hilo, kwa nini kuwa na wasiwasi juu ya yale mengine?
12:27 Angalieni maua jinsi yanavyomea. Hayafanyi kazi wala hayafumi. Hata hivyo, nawahakikishieni kwamba hata Solomoni mwenyewe na fahari zake zote hakupata kuvikwa vizuri kama ua mojawapo.
12:28 Lakini, kama Mungu hulivika vizuri jani la shambani ambalo leo liko na kesho latupwa motoni, je, hatawafanyia ninyi zaidi? Enyi watu wenye imani haba!
12:29 "Basi, msivurugike akili, mkihangaika daima juu ya mtakachokula au mtakachokunywa.
12:30 Kwa maana hayo yote ndiyo yanayohangaikiwa na watu wasiomjua Mungu. Baba yenu anajua kwamba mnahitaji vitu hivyo.
12:31 Shughulikieni kwanza Ufalme wa Mungu, na hayo yote mtapewa kwa ziada.
12:32 "Msiogope, enyi kundi dogo! Maana Baba yenu amependa kuwapeni Ufalme.
12:33 Uzeni mali yenu mkawape maskini misaada. Jifanyieni mifuko isiyochakaa, na jiwekeeni hazina mbinguni ambako haitapungua. Huko wezi hawakaribii, wala nondo hawaharibu.
12:34 Pale ilipo hazina yako, ndipo pia utakapokuwa moyo wako.
12:35 "Muwe tayari! Jifungeni mkanda kiunoni, na taa zenu ziwe zinawaka;
12:36 muwe kama watumishi wanaomngojea bwana wao arudi kutoka arusini, ili wamfungulie mara atakapobisha hodi.
12:37 Heri yao watumishi wale ambao bwana wao atakaporudi atawakuta wanakesha! Nawaambieni hakika, huyo bwana atajifunga mkanda kiunoni, atawaketisha mezani na kuwahudumia.
12:38 Heri yao watumishi hao ikiwa bwana wao atawakuta wanakesha hata ikiwa atarudi usiku wa manane au alfajiri.
12:39 Jueni kwamba, kama mwenye nyumba angejua saa ambayo mwizi atakuja, angekesha, wala hangeiacha nyumba yake ivunjwe.
12:40 Nanyi, kadhalika muwe tayari, maana Mwana wa Mtu atakuja saa msiyoitazamia."
12:41 Petro akamwambia, "Bwana, mfano huo ni kwa ajili yetu tu, au ni kwa ajili ya watu wote?"
12:42 Bwana akajibu, "Ni nani basi, mtumishi aliye mwaminifu na mwenye busara, ambaye bwana wake atamweka juu ya watumishi wake ili awape chakula wakati ufaao?
12:43 Heri yake mtumishi huyo ikiwa bwana wake atakaporudi atamkuta akifanya hivyo.
12:44 Hakika atampa madaraka juu ya mali yake yote.
12:45 Lakini, kama mtumishi huyo atafikiri moyoni mwake: na kusema: `Bwana wangu amekawia sana kurudi` halafu aanze kuwapiga watumishi wenzake, wa kiume au wa kike, na kula, kunywa na kulewa,
12:46 bwana wake atarudi siku asiyoitazamia na saa asiyoijua; atamkatilia mbali na kumweka fungu moja na wasioamini.*fb*
12:47 Mtumishi ambaye anajua matakwa ya bwana wake lakini hajiweki tayari kufanya anavyotakiwa, atapigwa sana.
12:48 Lakini yule afanyaye yanayostahili adhabu bila kujua, atapigwa kidogo. Aliyepewa vingi atatakiwa vingi; aliyekabidhiwa vingi zaidi atatakiwa kutoa vingi zaidi.
12:49 "Nimekuja kuwasha moto duniani, laiti ungekuwa umewaka tayari!
12:50 Ninao ubatizo ambao inanipasa niupokee; jinsi gani ninavyohangaika mpaka ukamilike!
12:51 Mnadhani nimekuja kuleta amani duniani? Hata kidogo; si amani bali utengano.
12:52 Na tangu sasa, jamaa ya watu watano itagawanyika; watatu dhidi ya wawili, na wawili dhidi ya watatu.
12:53 Baba atakuwa dhidi ya mwanawe, mwana dhidi ya baba yake; mama dhidi ya bintiye, binti dhidi ya mama yake; mama mkwe dhidi ya mke wa mwanawe na huyo dhidi ya mama mkwe wake."
12:54 Yesu akayaambia tena makundi ya watu, "Mnapoona mawingu yakitokea upande wa magharibi, mara mwasema: `Mvua itanyesha`, na kweli hunyesha.
12:55 Mnapoona upepo wa kusi unavuma, mwasema `Kutakuwa na hali ya joto` na ndivyo inavyokuwa.
12:56 Enyi wanafiki! Mnajua kutabiri hali ya hewa kwa kuangalia dunia na anga; kwa nini basi, hamwezi kujua maana ya nyakati hizi?
12:57 "Na kwa nini hamwezi kujiamulia wenyewe jambo jema la kufanya?
12:58 Maana kama mshtaki wako anakupeleka mahakamani, ingekuwa afadhali kwako kupatana naye mkiwa bado njiani, ili asije akakupeleka mbele ya hakimu, naye hakimu akakutoa kwa polisi, nao wakakutia ndani.
12:59 Hakika hutatoka huko nakwambia, mpaka utakapomaliza kulipa senti ya mwisho."
Created with FREE HTMLCompiler by Bibledatabase