MS Tech Home  /  BibleDatabase Home  /  Tell a Friend  / About MS Tech /Swahili New Testament Main Index

 

John 4

[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21]

4:1 Mafarisayo walisikia kwamba Yesu alikuwa anabatiza na kuwapata wanafunzi wengi kuliko Yohane.

4:2 Lakini ukweli ni kwamba Yesu hakuwa anabatiza ila wanafunzi wake.)

4:3 Basi, Yesu aliposikia hayo, alitoka Yudea akarudi Galilaya;

4:4 na katika safari hiyo ilimbidi apitie Samaria.

4:5 Basi, akafika Sukari, mji mmoja wa Samaria, karibu na shamba ambalo Yakobo alikuwa amempa mwanawe, Yosefu.

4:6 Mahali hapo palikuwa na kisima cha Yakobo, naye Yesu, kutokana na uchovu wa safari, akaketi kando ya kisima. Ilikuwa yapata saa sita mchana.

4:7 Basi, mwanamke mmoja Msamaria akafika kuteka maji. Yesu akamwambia, "Nipatie maji ninywe."

4:8 (Wakati huo wanafunzi wake walikuwa wamekwenda mjini kununua chakula.)

4:9 Lakini huyo mwanamke akamwambia, "Wewe ni Myahudi; mimi ni mwanamke Msamaria! Unawezaje kuniomba maji?" (Wayahudi hawakuwa na ushirikiano na Wasamaria katika matumizi ya vitu.)

4:10 Yesu akamjibu, "Kama tu ungalijua zawadi ya Mungu na ni nani anayekwambia: `Nipatie maji ninywe,` ungalikwisha mwomba, naye angekupa maji yaliyo hai."

4:11 Huyo mama akasema, "Mheshimiwa, wewe huna chombo cha kutekea maji, nacho kisima ni kirefu; utapata wapi maji yaliyo hai?

4:12 Au, labda wewe wajifanya mkuu kuliko babu yetu Yakobo? Yeye alitupa sisi kisima hiki; na yeye mwenyewe, watoto wake na mifugo yake walikunywa maji ya kisima hiki."

4:13 Yesu akamjibu, "Kila anayekunywa maji haya ataona kiu tena.

4:14 Lakini atakayekunywa maji nitakayompa mimi, hataona kiu milele. Maji nitakayompa yatakuwa ndani yake chemchemi ya maji ya uzima na kumpatia uzima wa milele."

4:15 Huyo mwanamke akamwambia, "Mheshimiwa, nipe maji hayo ili nisione kiu tena; nisije tena mpaka hapa kuteka maji."

4:16 Yesu akamwambia, "Nenda ukamwite mumeo uje naye hapa."

4:17 Huyo mwanamke akamwambia, "Mimi sina mume." Yesu akamwambia, "Umesema kweli, kwamba huna mume.

4:18 Maana umekuwa na waume watano, na huyo unayeishi naye sasa si mume wako. Hapo umesema kweli."

4:19 Huyo Mwanamke akamwambia, "Mheshimiwa, naona ya kuwa wewe u nabii.

4:20 Babu zetu waliabudu juu ya mlima huu, lakini ninyi mwasema kwamba mahali pa kumwabudu Mungu ni kule Yerusalemu."

4:21 Yesu akamwambia, "Niamini; wakati unakuja ambapo hamtamwabudu Baba juu ya mlima huu, wala kule Yerusalemu.

4:22 Ninyi Wasamaria mnamwabudu yule msiyemjua, lakini sisi tunamjua huyo tunayemwabudu, kwa maana wokovu unatoka kwa Wayahudi.

4:23 Lakini wakati unakuja, tena umekwisha fika, ambapo wanaoabudu kweli, watamwabudu Baba kwa nguvu ya Roho; watu wanaomwabudu hivyo ndio Baba anaotaka.

4:24 Mungu ni Roho, na watu wataweza tu kumwabudu kweli kwa nguvu ya Roho wake."

4:25 Huyo mama akamwambia, "Najua kwamba Masiha, aitwaye Kristo, anakuja. Atakapokuja atatujulisha kila kitu."

4:26 Yesu akamwambia, "Mimi ninayesema nawe, ndiye."

4:27 Hapo wanafunzi wake wakarudi, wakastaajabu sana kuona anaongea na mwanamke. Lakini hakuna mtu aliyesema: "Unataka nini?" au, "Kwa nini unaongea na mwanamke?"

4:28 Huyo mama akauacha mtungi wake pale, akaenda mjini na kuwaambia watu,

4:29 "Njoni mkamwone mtu aliyeniambia mambo yote niliyotenda! Je, yawezekana kuwa yeye ndiye Kristo?"

4:30 Watu wakatoka mjini, wakamwendea Yesu.

4:31 Wakati huohuo wanafunzi wake walikuwa wanamsihi Yesu: "Mwalimu, ule chakula."

4:32 Lakini Yesu akawaambia, "Mimi ninacho chakula msichokijua ninyi."

4:33 Wanafunzi wake wakaulizana, "Je, kuna mtu aliyemletea chakula?"

4:34 Yesu akawaambia, "Chakula changu ni kufanya anachotaka yule aliyenituma na kuitimiza kazi yake.

4:35 Ninyi mwasema: `Bado miezi minne tu, na wakati wa mavuno utafika!` Lakini mimi nawaambieni, yatazameni mashamba; mazao yako tayari kuvunwa.

4:36 Mvunaji anapata mshahara wake, na anakusanya mavuno kwa ajili ya uzima wa milele; hivyo mpandaji na mvunaji watafurahi pamoja.

4:37 Kwa sababu hiyo msemo huu ni kweli: `Mmoja hupanda na mwingine huvuna.`

4:38 Mimi nimewatuma mkavune mavuno ambayo hamkuyatolea jasho, wengine walifanya kazi, lakini ninyi mnafaidika kutokana na jasho lao."

4:39 Wasamaria wengi wa kijiji kile waliamini kwa sababu ya maneno aliyosema huyo mama: "Ameniambia mambo yote niliyofanya."

4:40 Wasamaria walimwendea Yesu wakamwomba akae nao; naye akakaa hapo siku mbili.

4:41 Watu wengi zaidi walimwamini kwa sababu ya ujumbe wake.

4:42 Wakamwambia yule mama, "Sisi hatuamini tu kwa sababu ya maneno yako; sisi wenyewe tumesikia, na tunajua kwamba huyu ndiye kweli Mwokozi wa ulimwengu."

4:43 Baada ya siku mbili Yesu aliondoka hapo, akaenda Galilaya.

4:44 Maana Yesu mwenyewe alisema waziwazi kwamba, "Nabii hapati heshima katika nchi yake."

4:45 Basi, alipofika Galilaya, Wagalilaya wengi walimkaribisha. Maana nao pia walikuwa kwenye sikukuu ya Pasaka, wakayaona mambo yote Yesu aliyotenda huko Yerusalemu wakati wa sikukuu hiyo.

4:46 Yesu alifika tena huko mjini Kana, mkoani Galilaya, mahali alipogeuza maji kuwa divai. Kulikuwa na ofisa mmoja aliyekuwa na mtoto mgonjwa huko Kafarnaumu.

4:47 Basi, huyo ofisa aliposikia kuwa Yesu alikuwa ametoka Yudea na kufika Galilaya, alimwendea akamwomba aende kumponya mtoto wake aliyekuwa mgonjwa mahututi.

4:48 Yesu akamwambia, "Msipoona ishara na maajabu hamtaamini!"

4:49 Huyo ofisa akamwambia, "Mheshimiwa, tafadhali twende kabla mwanangu hajafa."

4:50 Yesu akamwambia, "Nenda tu, mwanao yu mzima." Huyo mtu akaamini maneno ya Yesu, akaenda zake.

4:51 Alipokuwa bado njiani, watumishi wake walikutana naye, wakamwambia kwamba mwanawe alikuwa mzima.

4:52 Naye akawauliza saa mtoto alipopata nafuu; nao wakamwambia, "Jana saa saba mchana, homa ilimwacha."

4:53 Huyo baba akakumbuka kwamba ilikuwa ni saa ileile ambapo Yesu alimwambia: "Mwanao yu mzima." Basi, yeye akaamini pamoja na jamaa yake yote.

4:54 Hii ilikuwa ishara ya pili aliyoifanya Yesu alipokuwa anatoka Yudea kwenda Galilaya.

 

Created with  FREE HTMLCompiler by Bibledatabase