MS Tech Home  /  BibleDatabase Home  /  Tell a Friend  / About MS Tech /Swahili New Testament Main Index

 

John 18

[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21]

18:1 Yesu alipokwisha sema hayo, alikwenda ng`ambo ya kijito Kedroni, pamoja na wanafunzi wake. Mahali hapo palikuwa na bustani, naye Yesu akaingia humo pamoja na wanafunzi wake.

18:2 Yuda, aliyemsaliti Yesu, alipajua mahali hapo kwani mara nyingi Yesu alikutana na wanafunzi wake huko.

18:3 Basi, Yuda alichukua kikosi cha askari na walinzi kutoka kwa makuhani wakuu na Mafarisayo, akaja nao bustanini wakiwa na taa, mienge na silaha.

18:4 Yesu, hali akijua yote yatakayompata, akatokea, akawauliza, "Mnamtafuta nani?"

18:5 Nao wakamjibu, "Yesu wa Nazareti!" Yesu akawaambia, "Mimi ndiye." Msaliti Yuda alikuwa amesimama hapo pamoja nao.

18:6 Basi, Yesu alipowaambia: "Mimi ndiye", wakarudi nyuma, wakaanguka chini.

18:7 Yesu akawauliza tena, "Mnamtafuta nani?" Wakamjibu, "Yesu wa Nazareti!"

18:8 Yesu akawaambia, "Nimekwisha waambieni kwamba mimi ndiye. Basi, kama mnanitafuta mimi, waacheni hawa waende zao."

18:9 Alisema hayo ili yapate kutimia yale aliyosema: "Wale ulionipa sikumpoteza hata mmoja.")

18:10 Simoni Petro alikuwa na upanga; basi, akauchomoa, akamkata sikio la kulia mtumishi wa Kuhani Mkuu. Mtumishi huyo aliitwa Malko.

18:11 Basi, Yesu akamwambia Petro, "Rudisha upanga wako alani. Je, nisinywe kikombe alichonipa Baba?"

18:12 Kile kikosi cha askari, mkuu wake na walinzi wa Wayahudi walimkamata Yesu, wakamfunga

18:13 na kumpeleka kwanza kwa Anasi; Anasi alikuwa baba mkwe wa Kayafa ambaye alikuwa Kuhani Mkuu mwaka huo.

18:14 Huyo Kayafa ndiye aliyekuwa amewashauri Wayahudi kwamba ni afadhali mtu mmoja afe kwa ajili ya taifa.

18:15 Simoni Petro pamoja na mwanafunzi mwingine walimfuata Yesu. Huyo mwanafunzi mwingine alikuwa anajulikana kwa Kuhani Mkuu, hivyo aliingia pamoja na Yesu ndani ya ukumbi wa Kuhani Mkuu.

18:16 Lakini Petro alikuwa amesimama nje, karibu na mlango. Basi, huyo mwanafunzi mwingine aliyekuwa anajulikana kwa Kuhani Mkuu alitoka nje akasema na mjakazi, mngoja mlango, akamwingiza Petro ndani.

18:17 Huyo msichana mngoja mlango akamwuliza Petro, "Je, nawe pia ni mmoja wa wanafunzi wa mtu huyu?" Petro akamwambia, "Si mimi!"

18:18 Watumishi na walinzi walikuwa wamewasha moto kwa sababu kulikuwa na baridi, wakawa wanaota moto. Naye Petro alikuwa amesimama pamoja nao akiota moto.

18:19 Basi, Kuhani akamwuliza Yesu juu ya wanafunzi wake na mafundisho yake.

18:20 Yesu akamjibu, "Nimesema na kila mtu daima hadharani. Kila mara nimefundisha katika masunagogi na Hekaluni, mahali wakutanikiapo Wayahudi wote; na wala sijasema chochote kwa siri.

18:21 Kwa nini waniuliza mimi? Waulize wale waliosikia nini niliwaambia. Wao wanajua nilivyosema."

18:22 Alipokwisha sema hayo mlinzi mmoja aliyekuwa amesimama hapo akampiga kofi akisema, "Je, ndivyo unavyomjibu Kuhani Mkuu?"

18:23 Yesu akamjibu, "Kama nimesema vibaya, onyesha huo ubaya; lakini ikiwa nimesema vema, mbona wanipiga?"

18:24 Basi, Anasi akampeleka Yesu akiwa amefungwa, kwa Kuhani Mkuu Kayafa.

18:25 Petro alikuwa hapo akiota moto. Basi, wakamwuliza, "Je, nawe pia si mmoja wa wanafunzi wake?" Yeye akakana na kusema, "Si mimi!"

18:26 Mmoja wa watumishi wa Kuhani Mkuu, jamaa wa yule aliyekatwa sikio na Petro, akamwuliza, "Je, mimi sikukuona wewe bustanini pamoja naye?"

18:27 Petro akakana tena; mara jogoo akawika.

18:28 Basi, walimchukua Yesu kutoka kwa Kayafa, wakampeleka ikulu. Ilikuwa alfajiri, nao ili waweze kula Pasaka, hawakuingia ndani ya ikulu wasije wakatiwa najisi.

18:29 Kwa hiyo, Pilato aliwaendea nje, akasema, "Mna mashtaka gani juu ya mtu huyu?"

18:30 Wakamjibu, "Kama huyu hangalikuwa mwovu hatungalimleta kwako."

18:31 Pilato akawaambia, "Haya, mchukueni ninyi wenyewe, mkamhukumu kufuatana na Sheria yenu." Wayahudi wakamjibu, "Sisi hatuna mamlaka ya kumwua mtu yeyote."

18:32 Ilifanyika hivyo yapate kutimia maneno aliyosema Yesu kuonyesha atakufa kifo gani.)

18:33 Pilato akaingia tena ndani ya ikulu, akamwita Yesu na kumwuliza: "Ati wewe ndiye Mfalme wa Wayahudi?"

18:34 Yesu akamjibu, "Je, hayo ni maneno yako au wengine wamekwambia habari zangu?"

18:35 Pilato akamjibu, "Je, ni Myahudi mimi? Taifa lako na makuhani wamekuleta kwangu. Umefanya nini?"

18:36 Yesu akamjibu, "Ufalme wangu si wa ulimwengu huu. Kama ufalme wangu ungekuwa wa ulimwengu huu watumishi wangu wangenipigania nisitiwe mikononi mwa Wayahudi. Lakini sasa ufalme wangu si wa hapa."

18:37 Hapo Pilato akamwambia, "Basi, wewe ni Mfalme?" Yesu akajibu, "Wewe umesema kwamba mimi ni Mfalme. Mimi nimezaliwa kwa ajili hiyo; na kwa ajili hiyo nimekuja ulimwenguni kuwaambia watu juu ya ukweli. Kila mtu wa ukweli hunisikiliza."

18:38 Pilato akamwambia, "Ukweli ni kitu gani?" Pilato alipokwisha sema hayo, aliwaendea tena Wayahudi nje, akawaambia, "Mimi sioni hatia yoyote kwake.

18:39 Lakini, mnayo desturi kwamba mimi niwafungulie mfungwa mmoja wakati wa Pasaka. Basi, mwataka niwafungulieni Mfalme wa Wayahudi?"

18:40 Hapo wakapiga kelele: "La! Si huyu ila Baraba!" Naye Baraba alikuwa mnyang`anyi.

 

Created with  FREE HTMLCompiler by Bibledatabase