MS Tech Home  /  BibleDatabase Home  /  Tell a Friend  / About MS Tech /Swahili New Testament Main Index

 

John 15

[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13] [14] [15] [16] [17] [18] [19] [20] [21]

15:1 "Mimi ni mzabibu wa kweli, na Baba yangu ndiye mkulima.

15:2 Yeye huliondoa ndani yangu kila tawi lisilozaa matunda, na kila tawi lizaalo hulisafisha lipate kuzaa zaidi.

15:3 Ninyi mmekwisha kuwa safi kwa sababu ya ule ujumbe niliowaambieni.

15:4 Kaeni ndani yangu, nami nikae ndani yenu. Tawi haliwezi peke yake kuzaa matunda lisipokaa katika mzabibu hali kadhalika nanyi hamwezi kuzaa matunda msipokaa ndani yangu. ic

15:5 "Mimi ni mzabibu, nanyi ni matawi yake. Akaaye ndani yangu, nami ndani yake, huyo atazaa matunda mengi, maana bila mimi hamwezi kufanya chochote.

15:6 Mtu yeyote asipokaa ndani yangu hutupwa nje kama tawi litupwalo nje hata likakauka. Watu huliokota tawi la namna hiyo na kulitupa motoni liungue.

15:7 Mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, basi, ombeni chochote mtakacho nanyi mtapewa.

15:8 Baba yangu hutukuzwa kama mkizaa matunda mengi na kuwa wanafunzi wangu.

15:9 Mimi nimewapenda ninyi kama vile Baba alivyonipenda mimi. Kaeni katika pendo langu.

15:10 Mkizishika amri zangu mtakaa katika pendo langu, kama vile nami nilivyozishika amri za Baba yangu na kukaa katika pendo lake.

15:11 Nimewaambieni mambo haya ili furaha yangu ikae ndani yenu, na furaha yenu ikamilike.

15:12 Hii ndiyo amri yangu: pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi.

15:13 Hakuna upendo mkuu zaidi kuliko upendo wa mtu atoaye uhai wake kwa ajili ya rafiki zake.

15:14 Ninyi ni rafiki zangu mkifanya ninayowaamuru.

15:15 Ninyi siwaiti tena watumishi, maana mtumishi hajui anachofanya bwana wake. Lakini mimi nimewaita ninyi rafiki, kwa sababu nimewajulisha yote ambayo nimeyasikia kutoka kwa Baba yangu.

15:16 Ninyi hamkunichagua mimi; mimi niliwachagueni na kuwatuma mwende mkazae matunda, matunda yadumuyo, naye Baba apate kuwapa ninyi chochote mumwombacho kwa jina langu.

15:17 Basi, amri yangu kwenu ndiyo hii: pendaneni.

15:18 "Kama ulimwengu ukiwachukia ninyi, kumbukeni kwamba umenichukia mimi kabla haujawachukia ninyi.

15:19 Kama mngalikuwa watu wa ulimwengu, ulimwengu ungaliwapenda ninyi kama watu wake. Lakini kwa vile ninyi si wa ulimwengu, ila mimi nimewachagueni kutoka ulimwenguni, kwa sababu hiyo ulimwengu unawachukieni.

15:20 Kumbukeni niliyowaambieni: mtumishi si mkuu zaidi kuliko bwana wake. Ikiwa wamenitesa mimi, watawatesa na ninyi pia; kama wameshika neno langu, watalishika na lenu pia.

15:21 Lakini hayo yote watawatendeeni ninyi kwa sababu ya jina langu, kwani hawamjui yeye aliyenituma.

15:22 Kama nisingalikuja na kusema nao wasingalikuwa na hatia; lakini sasa hawawezi kujitetea kwamba hawana dhambi.

15:23 Anayenichukia mimi, anamchukia na Baba yangu pia.

15:24 Kama nisingalifanya kwao mambo ambayo hakuna mtu mwingine amekwisha yafanya wasingalikuwa na hatia; lakini sasa wameona niliyoyafanya wakinichukia mimi, wakamchukia na Baba yangu pia.

15:25 Na hivi ni lazima yatimie yale yaliyoandikwa katika Sheria yao: `Wamenichukia bure!`

15:26 "Atakapokuja huyo Msaidizi nitakayemtuma kwenu kutoka kwa Baba, huyo Roho wa kweli atokaye kwa Baba, yeye atanishuhudia mimi.

15:27 Nanyi pia mtanishuhudia kwa kuwa mmekuwa nami tangu mwanzo.

 

Created with  FREE HTMLCompiler by Bibledatabase