MS Tech Home  /  BibleDatabase Home  /  Tell a Friend  / About MS Tech /Swahili New Testament Main Index

 

Hebrews 5

[1] [2] [3] [4] [5]

5:1 Kila kuhani mkuu huchaguliwa kutoka miongoni mwa watu kwa ajili ya kumtumikia Mungu kwa niaba yao, kutolea zawadi na tambiko kwa ajili ya dhambi zao.

5:2 Maadamu yeye mwenyewe yu dhaifu anaweza kuwaonea huruma wale wasiojua kitu na wanaofanya makosa.

5:3 Na kwa vile yeye mwenyewe ni dhaifu, anapaswa kutolea dhabihu si tu kwa ajili ya watu, bali pia kwa ajili ya dhambi zake.

5:4 Hakuna mtu awezaye kujitwalia mwenyewe heshima ya kuwa kuhani mkuu. Kila mmoja huteuliwa na Mungu kuwa kuhani mkuu kama alivyokuwa Aroni.

5:5 Hali kadhalika naye Kristo hakujitwalia mwenyewe heshima ya kuwa kuhani mkuu, bali Mungu alimwambia: "Wewe ni Mwanangu; mimi leo nimekuwa baba yako."

5:6 Alisema pia mahali pengine: "Wewe ni kuhani milele, kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."

5:7 Yesu alipokuwa anaishi hapa duniani, kwa kilio kikuu na machozi, alisali na kumwomba Mungu ambaye alikuwa na uwezo wa kumwokoa kutoka kifo; naye alisikilizwa kwa sababu ya kumcha Mungu.

5:8 Lakini, ingawa alikuwa Mwana wa Mungu, alijifunza kutii kwa njia ya mateso.

5:9 Na alipofanywa mkamilifu, akawa chanzo cha wokovu wa milele kwa wale wote wanaomtii,

5:10 naye Mungu akamteua kuwa kuhani mkuu kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki.

5:11 Tunayo Mengi ya kusema juu ya jambo hili, lakini ni vigumu kuwaelezeni, kwa sababu ninyi si wepesi wa kuelewa.

5:12 Sasa mngalipaswa kuwa tayari walimu, lakini mnahitaji bado mtu wa kuwafundisheni mafundisho ya mwanzo ya ujumbe wa Mungu. Badala ya kula chakula kigumu, mnapaswa bado kunywa maziwa.

5:13 Kila anayepaswa kunywa maziwa huyo ni mtoto bado, hajui uadilifu ni nini.

5:14 Lakini chakula kigumu ni kwa ajili ya watu waliokomaa, ambao wanaweza kubainisha mema na mabaya.

 

Created with  FREE HTMLCompiler by Bibledatabase