MS Tech Home  /  BibleDatabase Home  /  Tell a Friend  / About MS Tech /Swahili New Testament Main Index

 

Galatians 5

[1] [2] [3] [4] [5] [6]

5:1 Kristo alitupa uhuru akataka tubaki huru. Basi, simameni imara wala msikubali tena kuwa chini ya nira ya utumwa.

5:2 Sikilizeni! Ni mimi Paulo ninayesema nanyi! Kama mkikubali kutahiriwa, Kristo hatawafaidia chochote.

5:3 Nasema tena wazi: kila anayekubali kutahiriwa itambidi kuishika Sheria yote.

5:4 Kama mnatazamia kukubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya Sheria, basi, mmejitenga mbali na Kristo; mko nje ya neema ya Mungu.

5:5 Kwa upande wetu, lakini, sisi tunatumaini kwamba kwa nguvu ya Roho tunakubaliwa kuwa waadilifu kwa njia ya imani.

5:6 Maana ikiwa tumeungana na Kristo Yesu, kutahiriwa au kutotahiriwa hakuna maana; cha maana ni imani ifanyayo kazi kwa mapendo. ic

5:7 Mwenendo wenu ulikuwa mzuri! Nani, basi aliyewazuia kuuzingatia ukweli?

5:8 Aliyesababisha hali hiyo si Mungu ambaye amewaiteni.

5:9 "chachu kidogo tu huchachusha donge lote la unga!"

5:10 Kutokana na kuungana kwetu na Bwana, nina tumaini kubwa kwamba ninyi hamtakuwa na msimamo tofauti nami. Tena yeyote huyo anayewavurugeni--awe nani au nani--hakika ataadhibiwa.

5:11 Na kwa upande wangu, ndugu zangu, kama bado ninahubiri kwamba kutahiriwa ni lazima, kwa nini basi, bado ninadhulumiwa? Kama ingalikuwa hivyo, mahubiri yangu juu ya msalaba wa Kristo yasingalileta aibu yoyote.

5:12 Laiti hao wanaowavurugeni wangejikatakata wenyewe!

5:13 Ninyi, ndugu, mliitwa muwe watu huru. Lakini uhuru huo usiwe kisingizio cha kutawaliwa na tamaa za kidunia; ila mnapaswa kutumikiana kwa upendo.

5:14 Maana Sheria yote hutimizwa katika kushika amri hii moja: "Mpende jirani yako kama unavyojipenda mwenyewe."

5:15 Lakini ikiwa mtaumana na kutafunana kama wanyama, jihadharini msije mkaangamizana wenyewe kwa wenyewe!

5:16 Basi, nasema hivi: mwenendo wenu na uongozwe na Roho, nanyi hamtafuata tena tamaa za kidunia.

5:17 Maana, tamaa za kidunia hupingana na matakwa ya Roho; na matakwa ya Roho hupingana na tamaa za kidunia. Mambo hayo mawili hayaafikiani; kwa sababu hiyo hamwezi kufanya yale mnayotaka ninyi wenyewe.

5:18 Kama mkiongozwa na Roho, basi, hamko tena chini ya Sheria.

5:19 Basi, matendo ya kidunia yanajulikana: uzinzi, uasherati, ufisadi;

5:20 kuabudu sanamu, uchawi, uadui, ugomvi, wivu, hasira, choyo, mabishano, mafarakano;

5:21 husuda, ulevi, ulafi na mambo mengine kama hayo. Nawaambieni tena kama nilivyokwisha sema: watu wanaotenda mambo hayo hawatakuwa na nafasi yao katika ufalme wa Mungu.

5:22 Lakini matokeo ya kuongozwa na Roho ni mapendo, furaha, amani, uvumilivu, wema, fadhili, uaminifu,

5:23 upole na kuwa na kiasi. Hakuna Sheria inayoweza kupinga mambo hayo.

5:24 Wale walio wa Kristo wameisulubisha hali yao ya kidunia pamoja na mawazo yake mabaya na tamaa zake.

5:25 Tukiishi kwa msaada wa Roho, na tuufuate mwongozo wake.

5:26 Basi, tusijivune, tusichokozane wala kuoneana wivu.

 

Created with  FREE HTMLCompiler by Bibledatabase