MS Tech Home  /  BibleDatabase Home  /  Tell a Friend  / About MS Tech /Swahili New Testament Main Index

 

Ephesians 2

[1] [2] [3] [4] [5] [6]

2:1 Ninyi mlikuwa mmekufa kwa sababu ya makosa na dhambi zenu.

2:2 Wakati ule mliishi kufuatana na mtindo mbaya wa ulimwengu huu, mkawa mnamtii mtawala wa pepo wenye nguvu wa anga, pepo ambao huwatawala sasa watu wasiomtii Mungu.

2:3 Na hata sisi sote tulikuwa kama wao; tuliishi kufuatana na tamaa zetu za kidunia na kufanya tu mambo yale yaliyoipendeza miili na akili zetu. Kidunia, sisi kama vile pia wao, tulistahili ghadhabu ya Mungu.

2:4 Lakini Mungu ni mwenye huruma nyingi. Alitupenda kwa mapendo yasiyopimika,

2:5 hata, ingawa tulikuwa tumekufa kwa sababu ya dhambi, alitufanya hai pamoja na Kristo. Kwa neema ya Mungu ninyi mmeokolewa.

2:6 Kwa kuungana na Kristo Yesu, Mungu alitufufua pamoja naye, tukatawale pamoja naye mbinguni.

2:7 Ndivyo alivyopenda kuonyesha kwa watu wa nyakati za baadaye, ukuu wa neema yake aliyotujalia kwa ukarimu katika kuungana kwetu na Kristo Yesu.

2:8 Maana, kwa neema ya Mungu mmekombolewa kwa njia ya imani. Jambo hili si matokeo ya juhudi zenu, bali ni zawadi ya Mungu.

2:9 Wala halitokani na matendo yenu wenyewe, asije mtu akajivunia kitu.

2:10 Sisi ni viumbe vyake Mungu, na kwa kuungana na Kristo Yesu, alituumba kwa ajili ya kuishi maisha ya matendo mema aliyotutayarishia tuyatende.

2:11 Ninyi mlio kwa asili watu wa mataifa mengine--mnaoitwa, "wasiotahiriwa" na Wayahudi ambao hujiita, "Waliotahiriwa," (kwa sababu ya kile wanachoifanyia miili yao)--kumbukeni mlivyokuwa zamani.

2:12 Wakati ule ninyi mlikuwa bila Kristo; mlikuwa nje ya jamii ya Israeli; mlikuwa wageni na hamkuwa na sehemu yoyote katika lile agano la zile ahadi. Mlikuwa bila matumaini Mungu hapa duniani.

2:13 Lakini sasa, kwa kuungana na Kristo Yesu, ninyi ambao hapo awali mlikuwa mbali, mmekaribishwa kwa njia ya damu yake Kristo.

2:14 Maana Kristo mwenyewe ametuletea amani kwa kuwafanya Wayahudi na watu wa mataifa mengine kuwa jamii moja. Kwa mwili wake yeye mwenyewe aliubomoa ule ukuta uliowatenganisha na kuwafanya maadui.

2:15 Aliiondoa ile Sheria ya Wayahudi pamoja na amri zake na kanuni zake, ili kutokana na jamii hizo mbili aumbe jamii moja mpya katika umoja naye na hivyo kuleta amani.

2:16 Kwa mwili wake, Kristo aliuangamiza uadui wao; kwa msalaba wake aliziunganisha jamii hizo kuwa moja na kuzipatanisha na Mungu.

2:17 Basi, Kristo alikuja akahubiri Habari Njema ya amani kwenu ninyi watu wa mataifa mengine mliokuwa mbali na Mungu, na pia kwa Wayahudi ambao walikuwa karibu na Mungu.

2:18 Hivyo, kwa njia yake, sisi sote, Wayahudi na watu wa mataifa mengine, tunaweza kumwendea Baba katika Roho mmoja.

2:19 Basi, ninyi si wageni tena, wala si watu wa nje; ninyi ni raia pamoja na watu wa Mungu, na ni watu wa jamaa ya Mungu.

2:20 Mmejengwa juu ya msingi uliowekwa na mitume na manabii, naye Kristo mwenyewe ndiye jiwe kuu la msingi.

2:21 Yeye ndiye mwenye kulitengeneza jengo lote na kulikuza hata liwe hekalu takatifu kwa ajili ya B wana.

2:22 Katika kuungana naye, ninyi pia mnajengwa pamoja na wote wengine, muwe makao ya Mungu kwa njia ya Roho wake.

 

Created with  FREE HTMLCompiler by Bibledatabase