MS Tech Home  /  BibleDatabase Home  /  Tell a Friend  / About MS Tech /Swahili New Testament Main Index

 

2 Peter 1

[1] [2] [3] [4] [5]

1:1 Mimi Simoni Petro, mtumishi na mtume wa Yesu Kristo, nawaandikia ninyi ambao, kwa wema wake Mungu wetu, na Mwokozi Yesu Kristo, mmejaliwa imani ileile ya thamani kuu tuliyojaliwa sisi.

1:2 Nawatakieni neema na amani tele katika kumjua Mungu na Yesu Bwana wetu.

1:3 Kwa uwezo wake wa kimungu, Mungu ametujalia mambo yote tunayohitaji, ili tuishi maisha ya kumcha Mungu kwa kumjua yeye aliyetuita tuushiriki utukufu na wema wake yeye mwenyewe.

1:4 Kwa namna hiyo ametujalia zawadi kuu na za thamani ambazo alituahidia, ili kwa zawadi hizo mpate kuziepa kabisa tamaa mbaya zilizomo duniani, na mpate kuishiriki hali yake ya kimungu.

1:5 Kwa sababu hiyo, fanyeni bidii ya kuongeza fadhila katika imani yenu: ongezeni elimu katika fadhila yenu,

1:6 kuwa na kiasi katika elimu yenu, uvumilivu katika kuwa na kiasi, uchaji wa Mungu katika uvumilivu wenu,

1:7 udugu katika uchaji wenu, na mapendo katika udugu wenu.

1:8 Mkiwa na sifa hizo zote kwa wingi, zitawawezesheni kuwa watendaji na kupata faida katika kumjua Bwana wetu Yesu Kristo.

1:9 Lakini mtu asiye na sifa hizo ni kipofu, hawezi kuona na amesahau kwamba alikwisha takaswa dhambi zake za zamani.

1:10 Kwa hiyo basi, ndugu zangu, fanyeni bidii zaidi kuufanya huo wito wenu mlioitiwa na Mungu uwe jambo la kudumu katika maisha yenu; kama mkiishi namna hiyo hamtaanguka kamwe.

1:11 Kwa namna hiyo mtafaulu kupewa haki kamili ya kuingia katika Utawala wa milele wa Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo.

1:12 Kwa hiyo nitaendelea kuwakumbusheni daima mambo haya, ingawa mmekwisha yafahamu, na mko imara katika ukweli mlioupokea.

1:13 Nadhani ni jambo jema kwangu, muda wote niishio hapa duniani, kuwapeni moyo na kuwakumbusheni juu ya mambo haya.

1:14 Najua kwamba karibu nitauweka kando mwili huu wenye kufa, kama Bwana alivyoniambia waziwazi.

1:15 Basi, nitajitahidi kuwapatieni njia ya kuyakumbuka mambo haya kila wakati, baada ya kufariki kwangu.

1:16 Wakati tulipowafundisheni juu ya ukuu wa kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, hatukutegemea hadithi tupu zisizo na msingi. Sisi tuliuona utukufu wake kwa macho yetu wenyewe.

1:17 Sisi tulikuwapo wakati alipopewa heshima na kutukuzwa na Mungu Baba, wakati sauti ilipomjia kutoka kwake yeye aliye Utukufu Mkuu, ikisema: "Huyu ni Mwanangu mpenzi, nimependezwa naye."

1:18 Tena, sisi wenyewe tulisikia sauti hiyo kutoka mbinguni wakati tulipokuwa pamoja naye juu ya ule mlima mtakatifu.

1:19 Tena, ujumbe wa manabii watuthibitishia jambo hilo; nanyi mwafanya vema kama mkiuzingatia, maana ni kama taa inayoangaza mahali penye giza mpaka Siku ile itakapopambazuka na mwanga wa nyota ya asubuhi utakapong`ara mioyoni mwenu.

1:20 Zaidi ya hayo, lakini, kumbukeni kwamba hakuna mtu yeyote awezaye kufafanua mwenyewe unabii ulio katika Maandiko Matakatifu.

1:21 Maana hakuna ujumbe wa kinabii unaotokana na matakwa ya binadamu, bali watu walinena ujumbe wa Mungu wakiongozwa na Roho Mtakatifu.

 

Created with  FREE HTMLCompiler by Bibledatabase