MS Tech Home  /  BibleDatabase Home  /  Tell a Friend  / About MS Tech /Swahili New Testament Main Index

 

2 Corinthians 1

[1] [2] [3] [4] [5] [6] [7] [8] [9] [10] [11] [12] [13]

1:1 Mimi Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na ndugu Timotheo, tunawaandikia ninyi mlio kanisa la Mungu huko Korintho, na watu wote wa Mungu kila mahali katika Akaya.

1:2 Tunawatakieni neema na amani kutoka kwa Mungu Baba yetu na Bwana Yesu Kristo.

1:3 Atukuzwe Mungu na Baba wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba mwenye huruma na Mungu mwenye kuleta faraja yote.

1:4 Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote, ili nasi tupate kuwafariji wengine katika kila taabu kwa faraja hiyohiyo tunayopokea kutoka kwa Mungu.

1:5 Naam, kadiri mateso ya Kristo yanavyozidi ndani yetu, ni kadiri hiyohiyo tunazidi kufarijiwa naye.

1:6 Ikiwa tunapata taabu, basi ni kwa ajili ya faraja na wokovu wenu. Tukifarijika, ni kwa ajili ya kuwafariji ninyi na kuwaunga mkono mpate nguvu ya kustahimili mateso yaleyale tunayoteseka sisi.

1:7 Tena, matumaini tuliyo nayo kwa ajili yenu ni imara; tunajua kwamba mkishiriki mateso yetu, mtashiriki pia faraja yetu.

1:8 Ndugu, tunataka kuwajulisheni taabu zilizotupata kule Asia; taabu hizo zilitulemea kupita kiasi, hata tukakata matumaini yote ya kuendelea kuishi.

1:9 Naam, tulikuwa kama watu waliohukumiwa kuuawa, ili tufundishwe kumtegemea Mungu mwenye kuwafufua wafu, badala ya kutegemea nguvu zetu sisi wenyewe.

1:10 Yeye alituokoa katika hatari kubwa ya kifo, na anaendelea kutuokoa; sisi tumemwekea tumaini letu kwamba atatuokoa tena,

1:11 ninyi mkiwa mnatuunga mkono kwa kutuombea. Hivyo neema tutakazokuwa tumepata kutokana na maombi ya watu wengi hivyo, ziwe sababu ya watu wengi zaidi kumshukuru Mungu kwa ajili yetu.

1:12 Sisi tunajivunia kitu kimoja: dhamiri yetu inatuhakikishia kwamba tumeishi ulimwenguni hapa, na hasa kati yenu, kwa unyenyekevu na unyofu tuliojaliwa na Mungu; hatukuongozwa na hekima ya kibinadamu bali neema ya Mungu.

1:13 Tunawaandikia ninyi mambo mnayoweza kuyasoma na kuyaelewa. Ninatumaini kwamba mtaelewa vizuri kabisa,

1:14 maana mpaka sasa mmenielewa kiasi fulani tu. Tunajua kwamba katika ile Siku ya Bwana Yesu mtaweza kutuonea sisi fahari kama nasi tunavyowaonea ninyi fahari.

1:15 Nikiwa na matumaini hayo, nilikusudia kuja kwenu hapo awali ili mpate baraka maradufu.

1:16 Nilikusudia kupita kwenu nikiwa safarini kwenda Makedonia, na wakati wa kurudi pia, ili nipate msaada wenu kwa safari yangu kwenda Yudea.

1:17 Je, mnadhani nilipopanga hivyo nimekuwa kama mtu asiye na msimamo? Je, mnadhani kwamba ninafanya uamuzi wangu kwa fikira za kibinadamu na kwamba nasema "Ndiyo" na "Siyo" papo hapo?

1:18 Mungu ni ukweli mtupu; basi, kile tulichowaambia ninyi si jambo la "Ndiyo" na "Siyo".

1:19 Maana Kristo Yesu, Mwana wa Mungu, ambaye mimi, Silwano na Timotheo, tulimhubiri kwenu, hakuwa mtu wa "Ndiyo" na "Siyo"; bali yeye daima ni "Ndiyo" ya Mungu.

1:20 Maana ndani yake ahadi zote za Mungu zimekuwa "Ndiyo". Kwa sababu hiyo, "Amina" yetu husemwa kwa njia ya Kristo kwa ajili ya kumtukuza Mungu.

1:21 Mungu mwenyewe ndiye mwenye kutuimarisha sisi na ninyi pia katika Kristo, na ndiye anayetuweka wakfu;

1:22 ndiye aliyetutia mhuri wa kuwa mali yake yeye na kutujalia Roho mioyoni mwetu kama dhamana ya mambo yote ambayo ametuwekea.

1:23 Mungu ndiye shahidi wangu--yeye anajua moyo wangu! Mimi sikuja tena Korintho, kwa sababu tu ya kuwahurumieni.

1:24 Hatutaki kutumia mabavu juu ya imani yenu; ninyi mko imara katika imani yenu. Wajibu wetu ni kufanya kazi pamoja kwa ajili ya furaha yenu.

 

Created with  FREE HTMLCompiler by Bibledatabase