MS Tech Home  /  BibleDatabase Home  /  Tell a Friend  / About MS Tech /Swahili New Testament Main Index

 

1 Timothy 4

[1] [2] [3] [4]

4:1 Roho asema waziwazi kwamba siku za baadaye watu wengine wataitupilia mbali imani; watazitii roho danganyifu na kufuata mafundisho ya pepo.

4:2 Mafundisho ya namna hiyo yanaenezwa na watu waongo wadanganyifu, ambao dhamiri zao ziko kama zimechomwa kwa chuma cha moto.

4:3 Watu hao hufundisha kwamba ni makosa kuona na pia kula vyakula fulani. Lakini Mungu aliviumba vyakula hivyo, ili wale walio waumini na ambao wanapata kuujua ukweli, wavitumie kwa shukrani.

4:4 Kila kitu alichoumba Mungu ni chema, wala hakuna kinachohitaji kukataliwa, bali vyote vipokelewe kwa sala ya shukrani,

4:5 kwa sababu neno la Mungu na sala hukifanya kitu hicho kikubalike kwa Mungu.

4:6 Kama ukiwapa ndugu wote maagizo haya, utakuwa mtumishi mwema wa Kristo Yesu, ukijiendeleza kiroho kwa maneno ya imani na mafundisho ya kweli, ambayo wewe umeyafuata.

4:7 Lakini achana na hadithi zile zisizo za kidini na ambazo hazina maana. Jizoeshe kuishi maisha ya uchaji wa Mungu.

4:8 Mazoezi ya mwili yana faida yake, lakini mazoezi ya kiroho yana faida za kila namna, maana yanatuahidia uzima katika maisha ya sasa, na pia hayo yanayokuja.

4:9 Usemi huo ni wa kusadikika kabisa na unastahili kukubaliwa.

4:10 Sisi tunajitahidi na kufanya kazi kwa bidii kwani tumemwekea tumaini letu Mungu aliye hai ambaye ni Mwokozi wa watu wote, na hasa wale wanaoamini.

4:11 Wape maagizo hayo na mafundisho hayo.

4:12 Usikubali mtu yeyote akudharau kwa sababu wewe ni kijana, lakini jitahidi uwe mfano kwa wanaoamini: katika usemi wako, mwenendo wako, upendo, imani na maisha safi.

4:13 Tumia wakati wako na juhudi yako katika kusoma hadharani Maandiko Matakatifu, kuhubiri na kufundisha, mpaka nitakapokuja.

4:14 Usiache kukitumia kile kipaji cha Kristo ndani yako ulichopewa kwa maneno ya manabii na kwa kuwekewa mikono na wazee.

4:15 Fikiri kwa makini juu ya hayo yote na kuyatekeleza kusudi maendeleo yako yaonekane na wote.

4:16 Angalia sana mambo yako mwenyewe, na mafundisho yako. Endelea kufanya hayo maana ukifanya hivyo utajiokoa mwenyewe na wale wanaokusikiliza.

 

Created with  FREE HTMLCompiler by Bibledatabase