MS Tech Home  /  BibleDatabase Home  /  Tell a Friend  / About MS Tech /Swahili New Testament Main Index

 

1 Timothy 2

[1] [2] [3] [4]

2:1 Kwanza kabisa, basi naomba dua, sala, maombi na sala za shukrani zitolewe kwa Mungu kwa ajili ya watu wote,

2:2 kwa ajili ya wafalme na wote wenye mamlaka, ili tupate kuishi maisha ya utulivu na amani pamoja na uchaji wa Mungu na mwenendo mwema.

2:3 Jambo hili ni jema na lampendeza Mungu Mwokozi wetu,

2:4 ambaye anataka watu wote waokolewe na wapate kuujua ukweli.

2:5 Maana yuko Mungu mmoja, na pia yuko mmoja anayewapatanisha watu na Mungu, binadamu Kristo Yesu,

2:6 ambaye alijitoa mwenyewe kuwakomboa watu wote. Huo ulikuwa uthibitisho, wakati ufaao ulipowadia.

2:7 Kwa sababu hiyo mimi nilitumwa niwe mtume na mwalimu wa watu wa mataifa, niutangaze ujumbe wa imani na ukweli. Nasema ukweli; sisemi uongo!

2:8 Basi, popote mnapokutana kufanya ibada nataka wanaume wasali, watu waliojitolea kweli na ambao wanaweza kuinua mikono yao wakisali bila hasira wala ubishi.

2:9 Hali kadhalika, nawataka wanawake wawe wanyofu na wenye busara kuhusu mavazi yao; wavae sawasawa na si kwa urembo wa mitindo ya kusuka nywele, kujipamba kwa dhahabu, lulu au mavazi ya gharama kubwa,

2:10 bali kwa matendo mema kama iwapasavyo wanawake wamchao Mungu.

2:11 Wanawake wanapaswa kukaa kimya na kuwa wanyenyekevu wakati wa kujifunza.

2:12 Mimi simruhusu mwanamke amfundishe au amtawale mwanamume; anapaswa kukaa kimya.

2:13 Maana Adamu aliumbwa kwanza, halafu Hawa.

2:14 Na wala si Adamu aliyedanganywa; bali mwanamke ndiye aliyedanganywa, akaivunja sheria ya Mungu.

2:15 Hata hivyo, mwanamke ataokolewa kwa kupata watoto, kama akidumu katika imani, upendo, utakatifu na unyofu.

 

Created with  FREE HTMLCompiler by Bibledatabase