MS Tech Home  /  BibleDatabase Home  /  Tell a Friend  / About MS Tech /Swahili New Testament Main Index

 

1 Peter 2

[1] [2] [3]

2:1 Basi, acheni uovu wote; uongo, unafiki, wivu na maneno ya kashfa visiweko tena.

2:2 Kama vile watoto wachanga wanavyotamani maziwa, nanyi pia mnapaswa kuwa na hamu ya maziwa halisi ya kiroho, ili kwa nguvu yake mpate kukua na kukombolewa.

2:3 Kama yasemavyo Maandiko Matakatifu: "Mmegundua kwamba Bwana ni mwema."

2:4 Basi, mwendeeni Bwana! Yeye ndiye jiwe hai lililokataliwa na watu; lakini mbele ya Mungu ni jiwe teule, na la thamani kubwa.

2:5 Mwendeeni yeye kama mawe hai mkajengeke na kuwa nyumba ya kiroho, ambamo mtatumikia kama makuhani watakatifu, kutolea dhabihu za kiroho zenye kumpendeza Mungu kwa njia ya Yesu Kristo.

2:6 Maana Maandiko Matakatifu yasema: "Tazama! Naweka huko sioni jiwe kuu la msingi, jiwe la thamani kubwa nililoliteua. Mtu atakayemwamini yeye aliye hilo jiwe, hataaibishwa."

2:7 Kwenu ninyi mnaoamini, jiwe hilo ni la thamani kubwa; lakini kwa wale wasioamini, "Jiwe walilokataa waashi, sasa limekuwa jiwe kuu la msingi."

2:8 Tena Maandiko yasema: "Jiwe hilo ni jiwe la kujikwaa, mwamba wa kuwaangusha watu." Watu hujikwaa kwa sababu hawauamini ule ujumbe; na ndivyo walivyopangiwa tangu mwanzo.

2:9 Lakini ninyi ni ukoo mteule, makuhani wa Mfalme, taifa takatifu; watu wake Mungu mwenyewe, mlioteuliwa kutangaza matendo makuu ya Mungu aliyewaiteni kutoka gizani akawaingizeni katika mwanga wake mkuu.

2:10 Wakati mmoja ninyi hamkuwa watu wa Mungu, lakini sasa ninyi ni watu wake; wakati mmoja hamkupewa huruma ya Mungu, lakini sasa mmeipokea.

2:11 Wapenzi wangu, nawasihi ninyi kama wageni na wakimbizi hapa duniani! Achaneni na tamaa za mwili ambazo hupingana na roho.

2:12 Mwenendo wenu kati ya watu wasiomjua Mungu unapaswa kuwa mwema kabisa, ili hata watakapowasingizieni kwamba mnatenda mabaya, waweze kutambua matendo yenu mema na hivyo wamtukuze Mungu Siku ya kuja kwake.

2:13 Basi, jiwekeni chini ya mamlaka yote ya kibinadamu, kwa ajili ya Bwana: utii kwa mfalme aliye mtawala mkuu,

2:14 utii kwa wakuu wa mikoa ambao wameteuliwa naye kuwaadhibu wahalifu na kuwasifu watendao mema.

2:15 Maana Mungu anataka mweze kuyakomesha maneno ya kijinga ya watu wasio na akili kwa matendo mema mnayofanya.

2:16 Ishini kama watu huru; lakini msiutumie uhuru wenu kuuficha ubaya, bali ishini kama watumishi wa Mungu.

2:17 Waheshimuni watu wote, wapendeni ndugu zenu waumini, mcheni Mungu, mheshimuni mfalme.

2:18 Enyi watumishi wa nyumbani, watiini wakuu wenu kwa heshima yote, wawe wema na wapole au wenye kuchukiza.

2:19 Maana kama mnavumilia maumivu ya mateso msiyostahili kwa sababu mwajua kwamba Mungu anataka hivyo, basi Mungu atawafadhili.

2:20 Maana, mtapata tuzo gani mkivumilia mapigo mnayostahili kwa sababu ya makosa yenu? Lakini kama mnavumilia mateso hata ingawa mmetenda mema, Mungu atawapeni baraka kwa ajili hiyo.

2:21 Hayo ndiyo mliyoitiwa; maana Kristo mwenyewe aliteseka kwa ajili yenu, akawaachieni mfano, ili muufuate mwenendo wake.

2:22 Yeye hakutenda dhambi, wala neno la udanganyifu halikusikika mdomoni mwake.

2:23 Alipotukanwa yeye hakujibu kwa tukano; alipoteseka yeye hakutoa vitisho, bali aliyaweka matumaini yake kwa Mungu, hakimu mwenye haki.

2:24 Yeye mwenyewe alizibeba dhambi zetu katika mwili wake juu ya msalaba, tupate kufa kuhusu dhambi, na kuishi kwa ajili ya uadilifu. Kwa majeraha yake, ninyi mmeponywa.

2:25 Ninyi mlikuwa kama kondoo waliokuwa wamepotea; lakini sasa mmemrudia Mchungaji na Mlinzi wa roho zenu.

 

Created with  FREE HTMLCompiler by Bibledatabase